NI NANI ANAMMEGEA
MWENZAKE MKATE?
“Kumegeana mkate si
kwa chakula tu, bali ni maisha yote ya taabu, furaha, na maisha yote kimwili na
kiroho”
Imani ni maisha ambayo ili yawe na maana kwetu
ni lazima tuyatafakari na kuyajadili kwa pamoja. Ni lazima kuelimishana na
kupeana mwanga, tusiamini kama Watoto wachanga bali tuamini kama watu wazima
wenye kuwajibika.
Imani ya Kikristo ina matukio makubwa mawili,
{a}kuzaliwa, na {b}kufa na kufufuka kwa Kristo.
“Alipoketi kula chakula pamoja nao, alichukua
mkate akabariki, akaumega, akawapa. Na macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua;
lakini yeye akatoweka kati yao” lk 24:30-31.
Luka katika sura ya 24:13-35
anaeleza kisa cha kushangaza kidogo baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Kisa kinatokea katika barabara ya kwenda Emau. Labda hii ni barabara ya
kiimani, maana hata Mtume Paulo, anakutana
na Kristo na kuwa mfuasi wake wa kweli katika barabara hii.
Katika barabara hiyo, Kristo aliwatokea Wafuasi
wawili, cha kushangaza ni kuwa ndugu hawa wawili hawakuweza kumtambua japo
walitembea naye na kuongea naye kwa muda juu ya matukio mbalimbali ya
Yerusalemu, na hasa tukio la kifo cha Kristo. Wakati wote huo waliokuwa
wakizungumza naye bado hawakuweza kumtambua, upo ushahidi kuwa hata baada ya
ufufuo bado Kristo alibaki katika sura ileile, hakubadilika. Tazama maandiko
katika luka 24:38-39, na Yohana 20:27.
Kutokana
na ushuhuda toka katika maandiko hayo, ni kweli kuwa Kristo alifufuka na mwili
wake. Lakini wale Wanafunzi wa Emau hawakuweza kumtambua. Inashangaza! {Lakini hii ilitokana na ukweli kuwa sura
ya Bwana Yesu iliharibika mno wakati wa mateso haingelikuwa rahisi kwa mtu
yeyote kumkumbuka tena} Ila walipomkaribisha ndani kwao wakati wa
chakula, alimega mkate akaanza kuwagawia, kwa tendo hilo wakamtambua, kwa nini
iwe hivyo?
Jibu pekee la kuondoa mashaka yote ni kwamba
kitendo cha kumegeana mikate, kitendo cha kukumbuka wengine kwanza, kitendo cha
kugawa chakula kwa wengine kwanza, kilifanywa na Kristo peke yake. Hiki ndicho
kitambulisho chake kikubwa. Vinginevyo hakuna, maelezo ya wafuasi wake
walioishinaye, wakasafiri naye na kusikiliza mahubiri yake, wamsahau na
kumkumbuka tu alipoumega mkate na kuwagawia wao kwanza.
Jamii ya wakati wa Yesu na jamii yetu leo ni
kuwa, mtu anakula kwanza kabla ya kuwakumbuka wengine, ni kwamba mikono
inaelekea kinywani kwanza kabla ya kuwagawia wengine. Kila mtu anashughulikia
uhai wake kwanza, kila mtu anatafuta mali zake kwanza, kila mtu anashiba
kwanza, katika jamii nyingi za kiafrika sehemu nzuri ya chakula alipewa baba na
ile inayobakia ndiyo ililiwa na mama na watoto; ndiyo maana wengine wanakula na
kusaza na wengine wanalala na kufa kwa njaa!
Uhakika wa hili kwanza tunaupata pale Kristo
alipofanya muujiza wa kuongeza mikate na samaki. Mitume walikuwa na chakula
chao, walitaka wale chakula chao, na wale waumini wengine waende kutafuta
chakula chao huko mjini: “Basi Yesu aliwaita wanafunzi wake akasema, ‘nawaonea
watu hawa huruma kwasababu kwa siku tatu wamekuwa nami, wala hawana chakula.
Sipendi kuwaacha waende bila kula wasije wakazimia njiani’, wanafunzi
wakamwambia, ‘hapa tuko nyikani, tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi
hivi? Yesu akawauliza “mnayo mikate mingapi?” wakamjibu, “saba na samaki
wachache”. Basi Yesu akaamuru watu waketi chini. Akaichukua ile makate saba na
wale samaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi nao wakawagawia
watu wote wakala, wakashiba…” Mathayo 15:32-37.
Saba ni namba takatifu, haina maana kwamba
walikuwa na mikate saba. Kwa maneno mengine mitume walitaka kusema walikuwa na
mikate ya kuwatosha wao tuna si ule umati wa watu, lakini Yesu alitaka umati
ule kwanza kabla ya mitume na yeye.
Hapa ndipo ujumbe na upekee wa Kristo Yesu
umelala; yaani kuwakumbuka wengine kabla yako wewe! Na mkate unayachukua maisha
yote. Mkate ni chakula, na chakula kinaleta uzima. Hivyo kumegeana mkate ni
kumegeana/kupeana uzima!
Matatizo ya dunia yetu yamelala hapa. Ni kwamba
katika hali ya kawaida, hali ambayo haina imani ya Kimungu, kila mtu
anajiangalia yeye kwanza, ashibe yeye kwanza, kila familia inajiangalia kwanza,
kila taifa linajiangalia kwanza kabla ya kuangalia usalama wa taifa jingine
kwanza. Umaskini, vita, na taabu zote za dunia yetu ni kwamba hatutaki
kumegeana mkate!
Baada ya kufundisha kwa muda wa miaka mitatu,
Yesu aliwaaaga mitume kwa fundisho ambalo linabeba ujumbe wake hapa duniani:
“halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema: “huu ndiyo mwili
wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka” luka
22:19.
Walipoandika injili hawatuambii kuwa Yesu
alikula kwanza. Tunachosoma ni kuwa alimega mkate na kuwapatia kwanza. Na akawaambia kwamba
wakitaka kumkumbuka na kukumbuka mafundisho yake, wamegeane mikate!
Wakati wa kanisa la kwanza, jumuiya nyingi za
Kikristo zilitambuliwa kwa kitendo cha kumegeana mikate. Hivyo na wafuasi wake
wale wa Emau walimtambua tu kwa kumega mkate, hawakumtambua kwa sura yake,
sauti yake au kitu kingine.
Kila mwaka tunaposheherekea Sikukuu ya Pasaka,
tunakumbwa na mafumbo ya kufa na kufufuka na fumbo la msalaba na kuuchukua kama
ishara yetu kubwa. Tunakumbwa na utamaduni wa kufanya sherehe hii kila mwaka,
ila hatuzami katika tafakuri ya ujumbe wa Kristo ya kumegeana mikate.
Ni nani anammegea jirani yake mkate? Katika katika
familia, katika Kanisa, na katika mitaa?